Sengerema kuzindua Sekondari mpya 11 mwakani
24 July 2024, 5:23 pm
Halmashauri ya Sengerema inatarajia kukamilisha ujenzi wa shule 11 mwakani na kuwa na jumla ya shule za Sekondari 46 waipongeza serikali ya awamu ya Sita
Na:Elisha Magege
Shule 11 mpya za Sekondari zinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu na kuanza kutumika Januari 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule hizo pamoja na ukarabati wa baadhi ya shule za msingi ,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Binuru Shekidele amesema kukamilika kwa shule hizo kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani sambamba na kupunguza kutembea umbali na utoro kwa wanafunzi.
Aidha Shekidele amemshukuru Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassani kwa kuendelea kuleta fedha za miradi ya elimu kwa wananchi wa Halmashauri ya Sengerema.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa Sekondari mpya ya Sogoso iliyopo kata ya Sima, na Igaka kata ya Buzilasoga ambazo zinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2024 shule zingine mpya za Sekondari ambazo zinaendelea kukamilishwa ni pamoja na Igulumuki, Isole, Chamabanda, Busulwangili, Kagunga, Nyitundu, Balatogwa, Kabusuri na Ilekanilo ambazo zinajengwa kwa fedha za Serikali kuu na baadhi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania na kukamilika kwa shule hizi kutaifanya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuwa na shule 46 za Sekondari.