Watoto waitaka serkali kukomesha ukatili unaoendelea nchini
17 June 2024, 7:28 am
Chimbuko la Maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Na:Emmanuel Twimanye
Watoto Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wameiomba Serikali kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea kushika kasi wilayani humo.
Hayo yamesemwa na watoto katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika wilayani yaliyofanyika katika shule ya Sekondari Mwabaluhi wakati wakisoma risala kwa mgeni rasmi na kusema kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto bado vinaendelea ikiwemo ubakaji ,ulawiti,ndoa za utotoni na utumikishwaji katika ajira hatarishi hali inayopelekea kukatisha ndoto zao za kielimu.
Afisa maendeleo ya jamii katika Halmshauri ya Wilaya ya Sengerema Yuster Mwambembe amewaomba watoto kutofumbia macho vitendo vya ukatili badala yake waendelee kuwafichua wanaowafanyia ukatili ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Naye katibu tawala wa Wilaya ya Sengerema Cathbeth Midala ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amewataka wazazi na walezi kutimiza jukumu la malezi kwa watoto ikiwa ni pamoja na kutimiza mahitaji yao ya msingi ili kufikia ndoto zao za kielimu.
Aidha kauli mbiu ya maadhimisho ya mtoto wa afrika kwa mwaka huu ni ‘’Elimu Jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi.