Moto wazuka na kuteketeza vitanda, magodoro Sengerema
21 May 2024, 7:49 pm
Matukio ya moto yameendelea kushika kasi katika Kata ya Tabaruka ambapo kwa siku za hivi karibuni bweni la wanafunzi wa kike shule ya sekondari Tamabu liliteketea kwa moto mara mbili huku chanzo cha tukio hilo kikiwa hakijafahamika mpaka sasa.
Na: Emmanuel Twimanye
Moto umezuka ghafla na kuteketeza vitu mbambali ikiwemo magodoro na vitanda katika nyumba ya mkazi mmoja wa kijiji cha Nyakato kata ya Tabaruka wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Akizungumzia tukio hilo mmiliki wa nyumba hiyo Paschal Kanyashi amesema kuwa wakati wanafamilia wote wakiwa nje moto huo ulizuka ghafla ndani ya nyumba hiyo na kuteketeza magodoro ,vitanda na nguo za wanafunzi.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamesikitishwa na tukio hilo na kueleza kuwa mara baada ya kutokea moto huo walifanikiwa kuuzima.
Mwenyekiti wa Kitingoji cha Nyakato Senta Deus Mabula amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwashukuru wananachi kwa kushirikiana kuzima moto huo .
Diwani wa kata ya Tabaruka Mh,Sospeter Busumabu ameliomba Jeshi la zima moto kufanya uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha moto huo na kwamba endapo mtu yeyote atakayebainika kuhusika katika tukio hilo hatua kali zichukuliwe dhidi yake .
Mkuu wa Jeshi la Zima moto Wilayani Sengerema Juma Ngwembe amewataka wananchi kuachana na matumizi ya mishumaa na vibatari badala yake watumie nishati ya jua ,taa za kisasa na umeme ili kukabiliana na matukio hayo ya moto.