DC Sengerema aongoza wananchi kupanda miti miaka 60 ya muungano
24 April 2024, 8:00 pm
Katika Zoezi hili la Kumbukizi ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jumla ya miche 800 imepandwa katika eneo la Hospitali ya Wilaya ya Sengerema sambamba na kufanya usafi katika Eneo hilo.
Na:Kelvin Philipo
Wananchi Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wametakiwa kuendelea kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na upandaji miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Wito huo umetolewa leo na mkuu wa wilaya ya Sengerema Senyi Ngaga wakati akiongoza zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Wilaya iliyopo katika kata ya Mwabaluhi ambapo miti Zaidi ya mia nane imepandwa kwa kushirikiana na viongozi pamoja na wadau mbalimbali wa mazingira.
Naye mhifadhi wa huduma za misitu Tanzania Wilayani Sengerema James Aloyce amesema suala la upandaji miti ni endelevu ilikulinda na kuhifadhi mazingira huku wakitarajia kufikisha MICHE laki mbili ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema Wilbard Bangora amesema watahakikisha miti hiyo inatunzwa kwa uangalifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo zoezi la upandaji miti linafanyika nchini kote kuelekea kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika April 26 mwaka huu.