Wanafunzi wachapwa viboko 75 kwa tuhuma za kufanya mapenzi shuleni
25 March 2024, 6:52 pm
Kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu mwilini pamoja na vifo ni matukio mbalimbali yaliyotendwa na yanayoendelea kutendwa dhidi ya wanafunzi huku sababu kubwa ikihusisha adhabu ya viboko jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa, utolewaji wa adhabu hizo haufuati taratibu, kanuni pamoja na miongozo husika iliyowekwa
Na:Emmanuel Twimanye
Wanafunzi 12 katika shule ya Sekondari Ipandikilo Iliyopo Kata ya Ngoma B Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wamedaiwa kuchapwa viboko 75 na baadhi ya walimu wa shule hiyo kwa tuhuma za kujihusisha na mapenzi shuleni.
Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya wanafunzi wakiwa katika kituo cha afya Ngoma B wamesema kuwa baada ya kutuhumiwa kujihusiha na mapenzi , walimu walianza kuwachapa viboko kwa zamu na kupelekea kupata maumivu makali sehemu mbalimbali za miili yao .
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaodaiwa kuchapwa viboko wamesikitishwa na tukio hilo na kuiomba serikali kuwaondoa shuleni hapo walimu walio tekeleza kitendo hicho.
Mkuu wa shule ya sekondari Ipandikilo Mwl, John Paul amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba wameshirikiana na afisa mtendaji wa kata hiyo kuwapeleka kwenye kituo cha afya wanafunzi hao kwa ajili ya kupatiwa matibabu wakati taratibu nyingine zikiendelea.
Mganga mfawidhi wa Kituo cha afya Ngoma B Abtwalib Nkwaje amethibitisha kuwapokea wanafunzi katika kituo hicho cha afya huku wakiwa na michubuko sehemu mbalimbali za milii yao.
Afisa mtendaji wa kata ya Ngoma B Emily John amekiri Ofisi yake kupokea malalamiko kuto0ka kwa wazazi wakiwa na watoto wao wakilalamikia kupewa adhabu zilizokithiri na kuchukua hatua za kumwita mkuu wa shule hiyo ili kutoa maelezo juu ya tukio hilo.
Diwani wa kata ya Ngoma B Mh,Donald Masindi amesema kuwa kitendo hicho hakiwezi kuvumiliwa na kushauri walimu wanaodaiwa kufanya kitendo hicho kuchuliwa hatua za kinidamu.
Kufuatia tukio hilo Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Sengerema Jackson Mazinzi na katibu wa Jumuiya hiyo Jamal Athuman wamewatembelea wanafunzi katika kituo hicho cha afya na kuagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mkuu wa shule hiyo ili kukomesha vitendo hivyo.
Kwa mjibu wa kanuni ya The Education (Corporal Punishment) Regulation G.N.294 ya mwaka 2002 inatoa mwongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani na kanuni ya 3 (1) inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhabu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima pia Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko 4 kwa tukio lolote.