CCM Sengerema yatatua mgogoro wa Ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 23
18 February 2024, 7:53 pm
Migogoro ya Ardhi wilayani Sengerema imekuwa Changamoto jambo lililoipelekea kamati ya Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi Sengerema kuanza kutembelea wananchi na kutatua ambapo imeanza na mgogo wa wananchi na Shule ya Msingi Kilabela uliodumu kwa zaidi ya miaka 23.
Na Emmanuel Twimanye
Wananchi waliodaiwa kuvamia eneo la shule ya Msingi Kilabela Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza na kuendesha shughuli za kilimo toka mwaka 2000 wameondolewa na ardhi hiyo kurejeshwa mikononi mwa shule hiyo.
Mgogoro huo umetatuliwa na katibu wa Jumuiya ya wazazi ya chama cha mapinduzi (CCM) Wilayani Sengerema Jamal Athumani baada ya kufika katika eneo hilo na kusikiliza pande zote mbili kati ya wananchi waliodaiwa kuvamia eneo hilo na uongozi wa shule hiyo .
Mwalimu mkuu aliyewahi kuhudumu katika shule ya msingi kilabela Deusdedith Magafu Majula amesema kuwa eneo la shule hiyo limetengwa toka mwaka 1993 na kuvamiwa na wananchi hao mwaka 2000 .
Diwani mstafu wa kata ya Sengerema ambaye kwa sasa ni katibu wa Mbunge wa Jimbo la Sengerema Levy Nghweli amesema kuwa eneo hilo ni mali halali ya shule .
Viongozi wa shule hiyo wamesema kuwa licha ya kulifikisha sakata hilo katika idara ya ardhi na vyombo vya dola lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa .
Diwani wa kata ya Nyatukala Mh,Michael Mchele na afisa mtendaji wa kata hiyo Hobokela Masukila wamewaomba wananachi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya shule .
Mmoja wa wananchi wanaodaiwa kuvamia eneo hilo aliyefahamika kwa jina moja la Mzee Masatu alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia suala hilo hakuwa na sababu za msingi za kujieleza.
Baadhi ya wananachi wameitaja idara ya ardhi kuwa ni chanzo cha kusababisha migogoro ya ardhi katika jamii kwa madai ya kupewa chochote na kuwatetea watu waliovamia maeneo huku wakimshukuru katibu wa jumuiya ya wazazi kwa kutatua mgogoro huo.
Naye Afisa ardhi wa Halmshauri ya wilaya ya Sengerema Saimon Mkalipa amekiri mgogoro huo kufikishwa katika idara hiyo na kwamba walikuwa wanaendelea kulishughulikia suala hilo.