Orkonerei FM
Orkonerei FM
17 February 2026, 2:03 pm

Wazazi na walezi wameaswa kuacha tabia ya kupakia picha za watoto wao kwenye mitandao ya kijamii, kwani hilo ni kosa la jinai linaloweza kuwafunga jela kwa miaka mitatu
Na Joyce Elius
Hayo yamesemwa Mapema leo kwenye kipindi cha Mchaka Mchaka na msaidizi wa kisheria kutoka shirika lisilo la kiserikali la SELA Bwana Hassan Fussa ambaye amesema vitendo hivyo vinasababisha madhara ya kisaikolojia na kiusalama yanayoweza kuwapata watoto hao sasa na hata ukubwani.
Amesema jambo hilo ni ukatili dhidi ya watoto, kwani linatoa mwanya kwa watu wenye nia ovu kufahamu maeneo walipo watoto na kuweza kuwadhuru kwa urahisi. Amebainisha kuwa baadhi ya watu wasio waaminifu hutumia picha hizo kujipatia fedha kwa njia za kitapeli, ikiwemo kudai kuwa mtoto anahitaji msaada wa matibabu wakati si kweli.
Sauti ya Bwana Hassan Fussa
Hassan Fussa amesisitiza kuwa picha zinazowekwa mtandaoni hubaki kwa muda mrefu na zinaweza kutumiwa vibaya, huku ikielezwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2022, kifungu cha 23, ambapo adhabu yake inaweza kuwa kifungo cha hadi miaka mitatu jela au faini ya shilingi milioni tano. Sheria hiyo inalinda haki na faragha ya mtu dhidi ya matumizi mabaya ya taarifa binafsi, huku wazazi wakikumbushwa kuwa na wajibu wa kulinda heshima na usalama wa watoto wao badala ya kufuata mkumbo wa kidijitali.
Sauti ya Bwana Hassan Fussa