Orkonerei FM
Orkonerei FM
31 January 2026, 12:26 pm

Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imetangaza mikakati mipya inayolenga kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, huku lengo kuu likiwa ni kupandisha kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 66 ya sasa hadi kufikia asilimia 85.
Na Isack Dickson
Akizungumza katika kikao kazi maalum kilichoandaliwa na Idara ya Elimu Awali, Msingi, na Sekondari, Mirerani Simanjiro Mkuu wa Idara hiyo, Mwalimu Darius Daudi Limandola, amesema kuwa Idara ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imekutana katika kikao kazi maalum kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina ya matokeo ya mitihani ya kitaifa ya mwaka 2025 na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha taaluma katika shule za awali, msingi, na sekondari ndani ya wilaya hiyo.
Mwalimu Darius ametaja sababu ambzo zinachangia matokea mabaya kwa wanafunzi Wilayani Simanjiro kuwa ni uhaba wa walimu, umbali mrefu wa kufuata huduma ya elimu na tishio la wanyamapori wakali kuwa miongoni mwa sababu zinazokwamisha ufaulu, huku ikitangaza mikakati mipya ikiwemo utoaji wa chakula cha mchana shuleni na ushirikishwaji wa viongozi wa dini na siasa ili kudhibiti utoro na kupandisha kiwango cha ufaulu hadi asilimia 85.
Aidha Mwalimu Darius, amewataka walimu wakuu na viongozi wa elimu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kujifunza mbinu bora na halali kutoka kwa shule zinazofanya vizuri ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.
Amesisitiza kuwa halmashauri hiyo imejikita katika kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu ngazi ya kata na shule, ikiamini kuwa mwalimu mkuu bora ndiye kiungo muhimu katika kutambua na kutatua changamoto za walimu, jambo ambalo litawezesha kufikia malengo ya kitaaluma kwa kuzingatia sheria, miongozo, na taratibu zilizopo.
Mwalimu Limandola amehitimisha kwa kutoa wito kwa wazazi, walezi, na jamii nzima ya Simanjiro kuendelea kushirikiana na uongozi wa elimu ili kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa. Amesema kuwa kwa kushikamana na kufuata miongozo ya serikali, wilaya hiyo itavuka kutoka ufaulu wa asilimia 66 wa sasa na kufikia asilimia 85, jambo litakaloinua hadhi ya taaluma katika halmashauri hiyo.
Pia, amewashukuru viongozi wa wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, na Mkurugenzi kwa kuendelea kuwaunga mkono katika jitihada za kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wa Simanjiro.