Orkonerei FM
Orkonerei FM
30 January 2026, 11:55 am
Na Nyangusi Olesang’ida

Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC) imevunja rekodi kwa kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 559 kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa hundi hizo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha DC, Baraka Simon Mesiaki, amebainisha kuwa jumla ya vikundi 29 vimenufaika, vikiwemo vikundi 15 vya wanawake, 12 vya vijana, na 2 vya watu wenye ulemavu. Mgawanyo huo umezingatia miongozo ambapo asilimia 4 imeenda kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana, na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arumeru, Noel Severe, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa usimamizi thabiti wa utekelezaji wa Ilani ya Chama unaowezesha wananchi kupata mikopo ya kujiendeleza kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi za zaidi ya shilingi milioni 500 kwa vikundi 29 katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Severe amewapongeza viongozi wa halmashauri hiyo, akiwemo Mwenyekiti na Mkurugenzi, kwa kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kuanzia ngazi ya kata.

Wakizungumza kwa hisia za matumaini na shukrani, wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuwajali wajasiriamali wadogo kupitia utoaji wa mitaji isiyo na riba. Wanufaika hao, ambao ni mchanganyiko wa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, wameeleza kuwa fedha hizo ni mkombozi utakaokwenda kuimarisha miradi yao ya ufugaji, kilimo, na biashara.
Kwa umoja wao, wanufaika hao wametoa shukrani za kipekee kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wa wilaya ya Arumeru kwa kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kwa uwazi.