Orkonerei FM

Mradi wa matangi waondoa adha ya maji Monduli

30 January 2026, 11:40 am

Na Nyangusi Olesang’ida

Picha ya Mbayani Tayai na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Monduli Kisioki Moitiko wakikabidhi vifaa vya matangi kwa kina mama

Katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa maji, taasisi ya Vijana Assembly imezindua mradi mkubwa wa kugawa matangi ya maji kwa wananchi wa wilaya ya Monduli, mradi unaolenga kurahisisha upatikanaji wa maji ya mvua na kuinua kipato cha kaya.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika kijiji cha Mtimmoja, Mkurugenzi wa Vijana Assembly, Mbayani Taiyai, ameeleza kuwa mradi huo umekuja kama mkombozi baada ya kubaini kuwa wananchi wengi walikuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kisioki Moitiko, ametoa pongezi za dhati kwa taasisi ya Vijana Assembly kwa hatua yake ya makusudi ya kuwaletea wananchi wa Monduli mradi wa matangi ya kuvuna maji ya mvua, akitaja kuwa ni mkombozi wa kweli dhidi ya ukame wa muda mrefu.

Akizungumza kwa hisia na furaha katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo uliogawa matangi ya lita 5,000, Mwenyekiti Kisioki alibainisha kuwa jitihada hizi ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya viongozi na wadau wa maendeleo.

Picha ya baadhi ya wanawake wa kijiji cha Mti Mmoja kata ya Sepeko Wilayani Monduli mkoani Arusha

Wanawake wa Monduli wameeleza kufurahishwa na mradi huu, wakidai kuwa utawaokoa na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji kwenye mabwawa ambayo si safi wala salama.

Naye mwananchi mwingine aliongeza kuwa, awali walikuwa wakitaabika sana na punda kufuata maji mbali, na kuiomba serikali na wadau kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwani bado kuna uhitaji mkubwa wa mabomba na miundombinu ya maji vijijini.