Orkonerei FM
Orkonerei FM
16 July 2025, 12:07 pm

Shule ya Sekondari Embooreet iliyopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara, inatumia bayogesi inayotokana na kinyesi cha wanafunzi kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia. Teknolojia hiyo, iliyosimikwa na Eclat Foundation kwa kushirikiana na Kamatec ya Arusha, imelenga kupunguza utegemezi wa kuni, kuimarisha usafi na kulinda mazingira.
Kwa zaidi ya wanafunzi 1,000, shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya kupika kwa kuni hasa wakati wa mvua. Kupitia mfumo wa bayogesi, kinyesi kutoka vyooni husafirishwa moja kwa moja hadi kwenye mtambo wa kuchakata, kisha gesi husambazwa jikoni kwa matumizi ya kupikia vyakula vya wanafunzi.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Hassani, amesema mfumo huu umepunguza gharama za kuni na kusaidia kuweka mazingira safi shuleni. Wanafunzi nao wameeleza kufurahishwa na mabadiliko haya yanayoendana na sera ya taifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, matumizi ya nishati safi yameongezeka kutoka asilimia 6 mwaka 2024 hadi 16 mwaka 2025, huku lengo ikiwa ni kufikia 80% ifikapo 2034.