CCM yazindua kampeni za udiwani Sengerema
11 March 2024, 6:03 pm
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza Uchaguzi Mdogo wa Madiwani Kata 23 Tanzania Bara, ukitarajiwa kufanyika tar 20 Machi 2024 Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Bw. Kailima, R. K jijini Dodoma tar15 Februari, 2024 miongoni mwa kata zilizotangazwa kufanya uchaguzi huo ni kata ya Buzilasoga iliyopo Halmashauri ya Sengerema.
Na:Emmanuel Twimanye.
Chama cha Mapinduzi (CCM ) Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza kimezindua kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Buzilasoga Wilayani Sengerema ili kuziba nafasi ya kiti hicho kilichoachwa wazi baada ya Diwani aliyekuwepo David Shilinde kufariki Dunia mwezi Septemba 28 2023.
Akizindua kampeni hizo mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Sengerema Mark Agustine Makoye amewataka wananchi kuchagua kiongozi bora atakayewaletea maendeleo na si vinginevyo.
Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mh,Hamis Tabasam amemuomba mgombea udiwani kata ya Buzilasoga kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM) Edina Godwin Bandihai endapo akichaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo kuhakikisha anatatua kero za wananchi ikiwemo uhaba wa maji .
Naye mgombea udiwani kata ya Buzilasoga kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi ( CCM) Edina Godwin Bandihai ameahidi kutatua kero za wananchi pindi atakapochaguliwa.
Aidha Jumla ya wagombea nane wa vya siasa wanachuana katika kinyang’anyiro cha udiwani kata ya Buzilasoga katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Machi, 20 mwaka 2024.
Wagombea waliopo katika kinyanganyiro hicho ni pamoja na Edina Godwin Bandihai (CCM), Deus Kabilondo Nkwabi (NLD), Mhoja Mathias Lubinza (ADC), Ramadhan Omary Said (UPDP), Saida Ramadhan Abdul (SAU), Rehema Hussein Khery (AAFP), Anna Sulwa Zengo (CCK) na Msafiri Joseph Nyamwitanga (Demokrasia Makini).