Walimu Sengerema wajikita kuchoma mkaa, kilimo badala ya kufundisha
22 January 2024, 6:40 pm
Shule ya msingi Mayuya ipo katika kata ya Tabaruka iliyopo Halmashauri ya Sengerema imekuwa ikifanya vibaya kwenye mitihani yake kutokana na changamoto ya Walimu wa shule hiyo kujikita katika shughuli zao binafsi za kuchoma mikaa na kilimo badala ya kufunsha.
Na;Emmanuel Twimanye.
Walimu wa shule ya Msingi Mayuya kata ya Tabaruka Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wamelalamikiwa kwa madai ya kushindwa kufundisha wanafunzi na kujikita katika shughuli za kilimo na uchomaji mkaa.
Malalamiko hayo yameibuliwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtunduni John Lubala Bushushu katika kikao cha maendeleo ya kata na kusema kuwa walimu wamekuwa wakijikita zaidi katika shughuli za kilimo na uchomaji mkaa hali iliyopekekea kushuka taaluma kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mayuya Ladslaus Zacharia amesema kuwa shule hiyo haiwezi kupata matokeo mazuri kwa kuwa wanafunzi wamekuwa wakilazimika kufanya mitihani sita ya kufunga muhula kwa siku moja kutokana na walimu kujikita katika shughuli zao binafsi.
Akitolea ufafanuzi suala la wanafunzi kufanya mitihani sita kwa siku moja afisa elimu wa kata ya Tabaruka Felister Nuge amesema kuwa kwa utaratibu Mwanafunzi anatakiwa kufanya mitihani mitatu kwa siku.
Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Mayuya Mwl,Seleman Maige ameahidi kuyafanyia kazi malalamiko hayo.
Kufuatia hali hiyo Diwani wa kata ya Tabaruka Mh,Sospeter Busumabu amewaagiza afisa elimu wa kata hiyo Ferister Nuge ,afisa mtendaji wa kata Sawia kimaro na afisa maendeleo Philipo kamfune kwenda katika shule hiyo kufanya kikao cha kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.