TANESCO wakata umeme chanzo cha maji Sengerema
3 July 2023, 12:29 pm
Kutokana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Sengerema SEUWASA kukabiliwa na malimbikizo ya deni la umeme kiasi cha shilingi milioni mia tatu, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekata huduma ya umeme katika chanzo cha maji kilichopo Nyamazugo.
Na: Emmanuel Twimanye
Wananchi mjini Sengerema mkoani Mwanza wamelazimika kutumia maji yasiyo safi na salama baada ya shirika la umeme Tanzania (TANESCO) wilayani humo kukata umeme kwa siku nne katika chanzo kikuu cha maji cha Nyamazugo kwa madai ya kushinikiza Wizara ya Maji kuwalipa deni lao la nyuma zaidi ya shilingi milioni mia tatu.
Wakizungumza na Radio Sengerema baadhi ya wananchi wamesema kuwa kwa sasa wanapata usumbufu mkubwa pindi wanapohitaji huduma muhimu ya maji.
Mbunge wa jimbo la Sengerema Mh. Hamis Tabasam amesikitishwa na wananchi kukatiwa huduma ya maji na kusema kuwa kwa sasa yupo jijini Dodoma kwa ajili ya kuzungumza na mamlaka husika ili kurejesha huduma hiyo.
Meneja utawala na rasilimali watu wa SEUWASA amekiri kukatiwa umeme na Tanesco katika chanzo cha maji na kwamba wanaendelea kuwasiliana na mamlaka za juu za kiutawala ili kutatua changamoto hiyo.
Hata hivyo meneja wa Tanesco wilayani Sengerema Martine Kilenga alipotafutwa na Radio Sengerema mara kadhaa ili kutolea ufafanuzi sakata hilo simu yake iliita bila kupokelewa.
Aidha tatizo la mji wa Sengerema kukatiwa umeme na wananachi kukosa huduma ya maji limekuwa likijitokeza mara kwa mara ambapo mpaka sasa halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu na mamlaka husika .