Sengerema FM

Akamatwa na jeshi la polisi kwa kumshushia kipigo mtoto mdogo

3 February 2023, 3:54 pm

Picha siyo ya tukio husika

Mama mlezi aliyemshambulia kwa kipigo kikali  mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya  Msingi Bukala  Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza    na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake  kwa madai ya kukojoa kitandani  hatimaye amekamatwa na jeshi la Polisi wilayani Sengerema.

Taarifa hiyo ya kukamatwa  kwa mama huyo na jeshi la polisi  imetolewa na afisa ustawi wa jamii  katika kituo cha afya Sengerema Consolatha Magaka wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini  kwake  na kusema kuwa tayari mama  huyo  amekamatwa na jeshi la polisi na kwamba mpaka sasa yupo mikononi mwa jeshi hilo kwa hatua zaidi za kisheria.

Baadhi ya wananchi  wilayani humo wamepongeza hatua ya jeshi la polisi ya kumakamata mama huyo  kwa kuwa litakuwa ni fundisho kwa akina mama wengine wenye tabia hiyo.

Viongozi wa dini wamewataka akina mama kuacha tabia ya kuwatesa watoto na badala yake wawalee katika maadili mema.

Naye afisa  tathimini na ufuatiliaji kutoka taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Tuwajali  inayojihusisha na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto Wilayani Sengerema John Kulindwa   amepongeza jeshi la polisi na vyombo vya habari  kwa kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili.

Ikumbukwe kuwa   Januari  18 mwaka huu  Radio Sengerema   iliripoti  habari ya  Mwanafunzi wa kike  mwenye umri wa miaka saba  anayesoma  Darasa la  kwanza katika shule ya Msingi Bukala Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ameshambuliwa kwa kipigo kikali na mama yake mlezi  na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake kwa madai ya kukojoa kitandani.

Taarifa ya mwandishi wetu Emmanuel Twimanye