Matukio ya mauaji ni hatari tuliombee Taifa-Sheikh JAH
13 September 2024, 7:07 am
Kufuatia kuwepo kwa matukio ya utekaji na mauaji ya raia nchini Tanzania viongozi wa Dini wazidi kuhimiza Waatanzania kila mmoja kwa imani yake kuliombea taifa ili Mungu atuepushe na majanga hayo.
Na;Emmanuell Twimanye
Wananachi Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wametakiwa kuliombea Taifa ili kukomesha matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali hapa nchini .
Kauli hiyo imetolewa na Shekh wa wilaya ya Sengerema ambaye pia ni Mwenyekiti wa amani Wilayani humo Ahmad Jah wakati akizungumza na Radio Sengerema kufuatia matukio ya utekaji na mauaji kukithiri na kuwaomba wananchi kila mmoja kwa imani yake kuliombea Taifa ili kukomesha matukio hayo.
Katika hatua nyingine amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaotekeleza vitendo hivyo.
Naye mwakilishi wa wenyeviti wa Serikali za mitaa Wilayani Sengerema Pelana Bagume kutoka mtaa wa Geita Road amesema kuwa kwa sasa matukio hayo yamezua taharuki kwa wananachi huku akiwaomba wazazi kuwa makini na watoto wao.
Baadhi ya wananachi wamesema kuwa kwa sasa wanaishi kwa hofu kubwa wakihofia usalama wa watoto wao na kuiomba serikali kukomesha matukio hayo.