Sengerema FM
Sengerema FM
20 November 2025, 11:36 am

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na Radio Sengerema hivi karibuni matukio ya watu kujiua yanaonesha kuongezeko kwa kasi katika wilayani Sengerema.
Na.Emmanuel Twimanye
Wananchi Wilayani Sengerema mkoani Mwanza, wametakiwa kuwa na hofu ya Mungu na kuacha kuchukua maamuzi ya kujiua kwa kujinyonga, ili kukomesha ongezeko la matukio hayo katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii katika Kituo cha Afya Sengerema, Bi.Consolatha Magaka, kufuatia kukithiri kwa wimbi la matukio ya wananchi kujinyonga na kupoteza maisha wilayani humo .
Katika hatua nyingine, Bi.Magaka amewasihi wanandoa kushirikishana watu wanaowaamini pindi wanapokumbana na changamoto za kifamilia, ili waweze kupata ushauri.
Baadhi ya wananchi, wamesema kinachopelekea wengi wao kushindwa kuweka wazi changamoto zinazowakabili ni kukosekana kwa usiri miongoni mwa ndugu, jambo linalowafanya kubaki na matatizo kwa kuhofia kufichuliwa.
Matukio ya kujiua yameendelea kushamiri katika Wilaya ya Sengerema ambapo katika kipindi cha wiki moja pekee, jumla ya watu watatu wamethibitishwa kupoteza maisha kutokana na kujitoa uhai.