

17 March 2025, 5:22 pm
Tanzania imeazimisha miaka minne tangu rais wa awamu ya Tano Dr. John Pombe Magufuli afariki Dunia,ambapo baadhi ya wananchi na viongozi wamesema wataendelea kumuenzi kiongozi huyo kwa uchapa kazi wake uliokuwa umetukuka kwani alifanikiwa pakubwa kurejesha nidhamu kazini.
Na,Emmanuel Twimanye
Watumishi wa serikali Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wametakiwa kuendelea kumuenzi kwa vitendo Hayati Dkt John Pombe Magufuli kwa kuchapa kazi kwa bidii , kupinga rushwa na kudumisha nidhamu kazini.
Hayo yamesemwa na Viongozi wa Dini Wilayani Sengerema wakati wakizungumza na Radio Sengerema Fm kuhusiana na kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii Wilayani Sengerema Stephano Mahozi amesema kuwa vitendo vya rushwa na kupungua kwa nidhamu ya watumishi kazini vinaendelea kushika kasi kwa sasa tofauti na utawala wa hayati Dkt John Pombe Magufuli .
Nao baadhi ya wazee wilayani humo wamesema kuwa baadhi ya viongozi wa serikali hawamuenzi hayati Dkt Magufuli kwa vitendo kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa na kushuka kwa nidhamu kazini .
Aidha Hayati Dkt. John Pombe. Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 Wilayani Chato Mkoa wa Geita na kufariki Dunia machi 17 mwaka 2021 kwa ugonjwa moyo .