Sengerema FM

Atupwa jela miaka 3 kwa kuwang’ata wenzie-Sengerema

18 February 2025, 5:47 pm

Amos John Malaki (30) katika katika aliyehukumiwa miaka 3 jela, akiwa chini ya uangalizi wa jeshi la polisi Mahakani Sengerema.Picha na Emmanuel Twimanye

Matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi wilayani Sengerema yanazidi kushika kasi, ambapo mtu mmoja amehukumiwa miaka 3 kwa kosa la kujeruhi watu wa wili na meno.

Na;Emmanuel Twimanye

Mahakama ya Wilaya Sengerema mkoani Mwanza imemhukumu kwenda jela miaka mitatu Mkazi wa Kijiji cha Soswa wilayani humo, Amos John Malaki  (30) baada ya kukutwa na hatia ya kuwajeruhi watu wawili kwa kuwang’ata.

Mshtakiwa amefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza  na kusomewa mashtaka hayo katika kesi hiyo ya Jinai namba 4079/2025 na kwa hiari yake bila kuisumbua mahakama amekiri kutenda makosa ya kuwajeruhi watu hao wawili.

Awali akisoma mashtaka Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nyamhanga Tissoro aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo Januari 08, 2025, Saa 5: 57 usiku kwa kumng’ata  Regina Thomas kwenye jicho. 

Katika tukio lingine lililotokea Januari 09,2025 Saa 6:01 usiku, mshtakiwa alimng’ata kidole gumba cha mkono wa kulia, Mashaka Idd Daudi aliyefika kuamua ugomvi na akakiondoa kabisa kinyume na vifungu vya 225 cha sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Amos Malaki ametiwa hatiani na mahakama hiyo baada ya kupitia vifungu vya sheria na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri zikiwemo PF3 za wahanga baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu pamoja na maelezo ya kukiri ya mtuhumiwa wakati akihojiwa kituo cha polisi ambayo pia hakuyapinga mahakamani yalipotolewa kama kielelezo, mahakama imejiridhisha bila ya kuacha shaka kwamba mtuhumiwa  alitenda makosa hayo licha ya ukili wake.

Alipopewa nafasi ya kujitetetea mbele ya mahakama hiyo mshtakiwa alieleza mahakama kuwa kilichopelekea yote hayo ni pombe na huyo mhanga wa pili aliingilia ugomvi usiomhusu baada ya kuona anagombana na mpenzi wake.

Baada ya kutiwa hatiani mshtakiwa aliiomba mahakama imuachilie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kudai kuwa alisababishiwa na pombe.

Hakimu, Kisoka amemhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama  hiyo.