Moses akutwa na baiskeli aliyoiba kanisani Sengerema
6 October 2024, 5:21 pm
Jamii imekua haiwaamini vijana kutokana na kuwa na tamaa ya mali za haraka jambo lililopelekea kuwa wadokozi na wezi wa vitu mbalimbali kwenye maeneo yao.
Na;Emmanuel Twimanye
Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 17 amekamatwa na Jeshi la Polisi jamii kata ya Misheni Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wakati akimuuzia Baiskeli mkazi wa kata hiyo aliyoiba katika kanisa la Parokia ya Yesu Kristo Mfalme Sengerema.
Akizungumzia tukio hilo akiwa chini ya ulinzi wa Polisi jamii kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Moses Emmanuel Nyanda amekiri kuiba Baiskeli hiyo kanisani hapo na kwenda misheni kuiuza ndipo alipokamatwa na Jeshi la Polisi jamii.
Mmiliki wa Baiskeli hiyo Faustine Chilimila amesema kuwa baada ya kumaliza misa ya kwanza hakuikuta baiskeli yake alipokuwa ameiegesha na muda mfupi alipigiwa simu akitaarifiwa kuwa kijana mmoja amekamatwa misheni akiwa na Baiskeli hiyo.
Mkazi wa misheni aliyetaka kuuziwa Baiskeli hiyo Masumbuko Costantine amesema kuwa wakati anauziwa Baiskeli na kijana huyo alimuomba kibali na kukosa ndipo alipomshtukia na kutoa taraifa kwa jeshi la polisi jamii na kufanikiwa kukamatwa.
Baadhi ya wananachi wa kata hiyo wamesikitishwa na tukio hilo na kuwaomba vijana kuacha kujihusisha na vitendo vya wizi.
Katibu wa Parokia ya Yesu Kristo Mfalme Sengerema Nichorous Chumus amekiri Baiskeli hiyo kuibiwa katika kanisa hilo na kuwaomba wazazi kuwalea vijana katika maadili mema.
Naye Kamanda wa Polisii jamii kata ya Misheni Rajabu Tunge amethibitisha kijana huyo kukamatwa na Jeshi hilo wakati akiuza Baiskeli hiyo na kuwaonya vijana kuacha kujihusisha na wizi.