RAS Mwanza akagua miradi itakayopitiwa na Mwenge 2024
17 September 2024, 7:01 pm
Halmashauri ya Sengerema inatarajia kuupokea Mwenge wa Uhuru tar 07/10 ukitokea Halmashauri ya Buchosa na kuukabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe tarehe 08 Oktoba, 2024.
Na;Elisha Magege
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amekagua jumla ya miradi saba itakayopitiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema pia amekagua ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya na jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Akikagua miradi hiyo, Katibu Tawala Mkoa ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuhakikisha wanafanyia kazi mapungufu yote yaliyobainika kwenye miradi hiyo kupitia ziara yake pamoja na kuweka sawa nyaraka za manunuzi na ujenzi wa miradi hiyo ili iweze kurahisisha ukaguzi wakati wa mbio za Mwenge.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukimbikizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema tarehe 07 Oktoba, 2024 ukitokea Halmashauri ya Buchosa ambapo ukiwa Halmashauri ya Sengerema unatarajia kupitia miradi saba yenye thamani ya shilingi bilioni 5, Miradi hiyo ni pamoja na Kuweka jiwe la Msingi la kituo cha Afya cha Nyamazugo, kuzindua mradi wa maji wa Chifunfu, kutembelea mradi wa utunzaji mazingira sekondari ya Ibondo, mradi wa vitalu vya miti wa vijana mjini Sengerema, jiwe la msingi la barabara za lami mjini Sengerema, huduma za afya hospitali ya Halmashauri Mwabaluhi pamoja na kuzindua shule mpya ya Msingi ya Isamilo.