Faustine akutwa amejinyonga chumbani kwake Sengerema
11 September 2024, 8:12 pm
Matukio ya vijana kujinyonga wilayani Sengerema yanazidi kushika kasi huku chanzo kikitajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi na ugumu wa maisha.
Na;Emmanuel Twimanye
Kijana mwenye umri wa miaka 34 aliyefahamika kwa jina la Faustine Malima amefariki Dunia kwa kujinyonga chumbani kwake katika Kitongoji cha Misheni Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ,huku chanzo cha tukio hilo kikiwa bado hakijafahamika.
Akizungumzia tukio hilo Magdalena Malima ambaye ni mdogo wake na marehemu amesema kuwa alipigiwa simu na mama yake akihitaji kuongea na Faustine na kumwagiza mtoto wake ampelekee simu ndani ndipo alipokuta amejinyonga na kupoteza maisha.
Baadhi ya majirani wa familia hiyo wamesikitishwa na tukio hilo na kuwaomba vijana kuacha kujichukulia maamuzi magumu ya kujitoa uhai.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Misheni Joseph Protas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tukio hilo limetokea leo majira ya saa tatu asubuhi na kuwataka vijana kuwashirikisha ndugu pindi wanapokutana na changamoto za maisha na si kuchukua maamuzi ya kujinyonga.
Aidha Jeshi la Polisi Wilayani Sengerema limefika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema.