Desemba 30,2024 Daraja la JPM ndani ya ziwa Victoria kuanza kazi
4 July 2024, 9:00 am
Daraja la JP.Magufului ni daraja refu kuliko madaraja yote Afrika mashariki na limetumia teknolojia ya madaraja marefu (Long Span Bridges), inayoitwa “Extra Dosed Bridge” kukamilika kwake litakuwa kivutio cha utalii Nchini na ukanda wa afrika mashariki kwa ujumla.
Na;Elisha Magege
Daraja la J.P. Magufuli (Kigongo – Busisi) lenye urefu wa Kilomita 3.0 na barabara unganishi Kilomita 1.66 linatarajiwa kuanza kutumika Tarehe 30 Disemba 2024 likiunganisha Barabara Kuu ya Usagara – Sengerema – Geita zenye urefu wa Kilomita 90.
Akizungumza baada ya kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa daraja hilo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza Mhandisi Paschal Ambrose amesema kuwa daraja hilo linajengwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation ikishirikiana na China Railway 15 Bureau Group Corporation (CCECC – CR15G JV) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 592.6 bila 18% VAT.
Mhandisi Ambrose amezitaja faida zitakazopatikana baada ya kukamilika kwa daraja hilo kuwa ni pamoja na kupunguza muda wa kusafiri na uwepo wa uhakika wa usafiri masaa 24, kuondoa msongamano wa magari uliokuwa unatokea kwenye feri, Litakuwa kiungo muhimu kwa Mkoa wa Mwanza na Mikoa inayouzunguka pamoja na Nchi Jirani na pia Daraja hilo litakuwa kivutio muhimu kwa Mkoa wa Mwanza na ni nembo kwa nchi ya Tanzania.
Daraja hilo linajengwa Urefu wa kilometa 3.0 Upana meta 28.45; unaojumuisha njia mbili (2) za Magari (Carriageways) zenye upana wa meta 7.0 kila upande, njia ya maegesho ya dharura meta 2.5 kila upande, njia za watembea kwa miguu (Walkways) meta 2.5 kila upande, eneo la kati linalotenganisha uelekeo tofauti wa barabara (Median) meta 2.45, kingo za magari (GuardRails Kerbs) meta 0.5 kila upande, na kingo za watembea kwa miguu (HandRails Kerbs) meta 0.5 kila upande.