Akatwa mapanga usiku akienda kwenye mkesha wa pasaka
2 April 2024, 3:13 pm
Mtu asiyejulikana amemjeruhi kwa mapanga mwanamke anayejulikana kwa majina ya Mariam Sebagi mkazi wa mtaa wa Misheni usiku akiwa na wenzake wakielekea kwenye mkesha wa Pasaka mjini Sengerema.
Na:Emmanuel Twimanye
Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Mariam Sebagi mkazi wa mtaa wa Misheni wilayani Sengerema mkoani Mwanza amedaiwa kushambuliwa kwa mapanga na mtu asiyejulikana na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake, huku chanzo cha tukio hilo kikiwa bado hakijafahamika .
Akizungumzia tukio hilo mwanamke huyo akiwa amelazwa katika Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema amesema kuwa wakati anakwenda kwenye mkesha wa pasaka na wenzake ndipo alitokea ghafla mtu asiyejulikana na kuanza kumshambulia kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake
Baadhi ya ndugu na majirani wa familia hiyo wamesikitishwa na kulaani vikali tukio hilo huku wakiiomba serikali kufanya uchaguzi wa tukio hilo ili kubaini mtu aliyefanya kitendo hicho cha kinyama na kumchukulia hatua kali za kisheria.
Nesi muuguzi katika Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema Tabu Makelemo amekiri kumpokea mwanamke huyo katika Hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu huku akiwa amepoteza fahamu ambapo kwa sasa hali yake inaendelea vizuri.
Naye mwenyekiti wa Mtaa wa Misheni Joseph Protas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kushirikiana na jeshi la polisi kumtafuta mtu anayedaiwa kutenda tukio hilo .
Hata hivyo Jeshi la polisi Wilayani Sengerema limefika eneo la tukio na kushirikiana na ndugu kumbeba mwanamke huyo kisha kumpeleka katika Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema kwa ajili ya kupatiwa matibabu.