Fisi aua mtoto wa miaka 9, ajeruhi mwingine Sengerema
13 March 2024, 7:09 pm
Matukio ya watoto kushambuliwa na fisi wilayani Sengerema yamezidi kushamili maeneo mbalimbali ambapo akizungumza katika Baraza la Madiwani hivi karibuni Diwani wa kata ya Chifunfu Robert Madaha alidai kuwa fisi waliopo Sengerema wanamilikiwa na watu kwani wana majina na namba za usajili kama pikipiki.
Na: Emmanuel Twimanye
Mtoto mwenye umri wa miaka tisa katika Kitongoji cha Izengabasumba kijiji cha Nyamahona kata ya Kasenyi wiayani Sengerema mkoani Mwanza amefariki dunia kwa kushambuliwa na fisi wakati anakienda kuchanja kuni mlimani na wenzake.
Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya ndugu na wananchi wa kijiji hicho wamesikitishwa na tukio hilo na kueleza kuwa wakati mtoto huyo anakwenda mlimani na wenzake kuchanja kuni walimwona fisi ambapo wenzake walifanikiwa kukimbia ndipo fisi huyo alipomkamata kisha kukimbia naye mlimani.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Izengabasumba Paul Shingashinga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaomba wazazi kuacha kuwatuma watoto nyakati za usiku ili kunusuru maisha yao.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Nyamahona Yasinta Costantine Fabiani amesema kuwa kijiji hicho kina mkakati wa kuwaleta wataalam kwa ajili ya kutokomeza wanayama hao ambao wamekuwa tishio kwa maisha ya binadamu.
Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Kasenyi Asteria Ngalula amekiri kupoteza maisha kwa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Pendo Kulwa kwa kushambuliwa na fisi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Naye afisa Wanyamapori Msaidizi mkoani Mwanza Godfrey Baisi amekiri kupokea taarifa zukio hilo na kusema kuwa tayari ametuma kikosi kwa ajili ya kwenda kuwawinda fisi hao.
Aidha matukio ya watu kushambuliwa na fisi yameendelea kuripotiwa mara kwa mara bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu wilayani Sengerema, huku yakisababisha vifo na ulemavu kwa baadhi ya wananchi.