Fisi Maria14 avuruga kikao cha madiwani Sengerema
3 March 2024, 6:58 pm
Kufuatia kuwepo kwa changamoto ya wanyama fisi katika kata ya Chifunfu iliyopo Halmashauri ya Sengerema mkoani Mwanza Diwani wa kata hiyo Robert Madaha amelifikisha jambo hili kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ambapo limeibua hisia mpya baada ya kuonekana baadhi ya fisi wana majina, shanga na namba za usajili.
Na;Emmanuel Twimanye
Fisi sita akiwemo aliyekuwa ameandikwa jina la Maria namba 14 akiwa amevaa heleni na wengine waliokuwa wamevaa shanga wameuawa na wataalam wa jadi katika kijiji cha Chifunfu kata ya Chifunfu wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Hayo yamebainishwa na Diwani wa kata ya Chinfunfu Madaha katika mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmahauri ya Wilaya ya Sengerema na kusema kuwa fisi na mamba wamekuwa tishio katika kata hiyo na kuiomba serikali kuingilia kati suala hilo.
Baadhi ya wananchi wameshangazwa na tukio hilo na kuiomba jamii kumrudia Mwenyezi Mungu .
Kufuatia hatua hiyo Mkuu wa wilaya ya Sengerema Mh,Senyi Ngaga amemuomba Diwani wa kata ya Chifunfu kukaa na wazee ili kulitafutia ufumbuzi suala hilo huku akiwaomba wananachi kuwa makini dhidi ya wanayama hao.
Aidha matukio ya fisi na mamba yameendelea kushika kasi wilayani Sengerema na kupelekea vifo kwa binadamu huku wengine wakiachwa na ulemavu licha ya serikali kuendelea kukabiliana na wanyama hao.