Mlinzi achinjwa na watu wasiojulikana usiku Sengerema
30 January 2024, 2:32 pm
Matukio ya walinzi kuuawa mjini Sengerema yamekuwa yakijirudia mara kwa mara kila mwaka jambo hili limekuwa likihusishwa na imani za kishirikina pamoja na wivu wa kimapenzi.
Na;Said Mahera
Mtu mmoja anaesadikiwa kuwa ni mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya Mwasenda aliyekuwa akilinda katika ukumbi wa starehe wa Nchemenche Pub uliopo mtaa wa Migombani kata ya Nyampulukano Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza,ameuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.
Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesikitishwa na mauaji hayo ya kinyama, na kuiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina kwa kushilikiana na jamii kuwabaini watu waliofanya kitendo hicho, na kuwachukulia hatua kali za kisheria ili kukomesha ukatili huo.
Mmiliki wa ukumbi wa Nchemenche Sylvester Nchemenche amesikitishwa na tukio hilo huku akiviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini watu waliotekeleza unyama huo.
Nae mwenyekiti wa mtaa wa Migombani Antony Busumabu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo na kutaja jina la mlinzi ambae ameuawa kuwa ni Ghati Lioba Chacha mwenye umri wa miaka 35 .
Hata hivyo Jeshi la Polisi Wilayani Sengerema limefika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema .