Akatwa panga na mpwa wake kisa deni la elfu 80
18 January 2024, 4:47 pm
Matukio ya ndugu wa familia kuuana na kujeruhiana kisa mali yamekuwa yakitajwa zaidi nchini ambapo katika wilaya ya sengerema mnamo mwezi October.2023 mtu mmoja aliuwawa na ndugu zake katika kijiji cha Ilunda kata ya Ngoma wakigombania shamba la urithi, Vivyo kwa mzee Manyema Marco ambaye amekatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na mtoto wa dada yeke kisa ni kumdai fedha alizomkopesha zenye thamani ya elf.80.
Na;Emmanuel Twimanye.
Mzee mwenye umri wa miaka 61 katika Mtaa wa Kizugwangoma Kata ya misheni Wilayani Sengerema amedaiwa kushambuliwa kwa mapanga na rungu na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake wakati akidai deni la shilingi elfu themanini kwa ndugu yake.
Akizungumzia tukio hilo mzee huyo aliyefahamika kwa majina ya Manyema Marco amesema kuwa alimkopesha mpwa wake shilingi elfu themanini mwaka jana ambapo alipokwenda nyumbani kwake kumdai ndipo aliposhambuliwa kwa mapanga na rungu kichwani na miguuni.
Mke wa mzee huyo Skolastica Elias Makanyaga amesikitishwa na tukio hilo na kushangzawa na kitendo cha ndugu yake kumshambulia mme wake bila hatia.
Baadhi ya majirani wa familia hiyo wameiomba serikali kumtafuta mwanaume aliyedaiwa kumshambulia mzee huyo na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kizugwangoma Kwiligwa Methusela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Jeshi la Polisi Wilayani Sengerema limefika eneo la tukio na kumchukua mzee aliyeshambuliwa kisha kumpeleka katika Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema kwa ajili ya kupatiwa matibabu wakati likiendelea kumtafuta mwanaume anayedaiwa kufanya tukio hilo ambaye ametokomea kusikojulikana.