Mwanamke akutwa amefariki kitandani kwake
9 January 2024, 8:43 am
Matukio ya watu kukutwa wamefariki Dunia yanazidi kushika kasi wilayani Sengerema ambapo baadhi yao wanadai yanasababishwa na msongo wa mawazo pamoja na ugumu wa maisha kwa watu jambo lililopelekea mwenyekiti wa mtaa wa Migombani wilayani hapo kuwataka wananchi kuwa na tabia ya kujuliana hali asbuhi kila siku kabla ya kwenda kwenye majukumu yao.
Na:Emmanuel Twimanye.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 41 amekutwa akiwa amefariki kitandani katika mtaa wa migombani kata ya Nyampulukano Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza huku chanzo cha tukio hilo kikiwa hakijafahamika.
Mashuhuda ,mmiliki wa nyumba na majirani wamesema kuwa wamebaini tukio hilo baada ya kijana mmoja anayefanya kazi na mme wa marehemu Simon Mathias kufika nyumbani hapo majira ya saa mbili na nusu asububi akimtafuta na kwamba walipobisha hodi katika chumba chake ilisikika sauti ya mtoto akimwita mama yake ndipo walipolazimika kuingia ndani na kukuta mwanamke huyo yuko kitandani akiwa amefariki Dunia.
Balozi wa eneo hilo Peragia Tete amesema kuwa taarifa za tukio hilo amezipata kutoka kwa mmiliki wa nyumba aliyokuwa amepanga mwanamke huyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Migombani Anton Busumabu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutaja jina la mwanamke aliye kutwa akiwa amefariki Dunia kuwa ni Martina Patrick Misalaba huku akiwataka wananachi kujenga tabia ya kujuliana hali hususani nyakati za asubuhi.
Jeshi la Polisi Wilayani Sengerema limefika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.