Azua taharuki akidhaniwa kuwa mchawi kanisani
30 October 2023, 9:10 pm
Matukio ya watu kudhaniwa kuwa wachawi yamezidi kushika kasi wilayani Sengerema ambapo mwanzoni mwa mwaka huu 2023 wanawake wanne waliodhaniwa kuwa ni wachawi walikamatwa eneo la Mwabaruhi mjini Sengerema.
Na:Emmanuel Twimanye.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida , Mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30, anayesadikiwa kuwa ni mchawi amekwama ndani ya kanisa la Ebezeza Wilayani Sengerema wakati akidaiwa kujaribu kufanya jaribio la kishirikina.
Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamesikitishwa na tukio hilo na kusema kuwa awali alifika mbwa kanisani hapo na kumfukuza na kwamba wakati ibaada inaelekea mwishoni ghafla mwanamke huyo alitua kanisani akiwa na chungu ,konono na vitu vinavyosadikiwa kuwa ni dawa kwenye mkoba wake kisha kuanza kumshambulia mchungaji.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wameshangazwa na tukio hilo na kuishauri jamii kuachana na vitendo vya Imani za kishirikina kwa kuwa vinarudisha nyuma maendeleo.
Mchungaji wa Kanisa la Ebeneza Ashery Olongai amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuiomba jamii kuachana na masuala ya Imani za kishirikina na kumrudia mwenyezi Mungu.
Hata hivyo mwanamke huyo hajafahamika ni mkazi wa wapi ambapo hadi sasa amezuiliwa katika kanisa hilo kwa ajili ya hatua zaidi.