Ukimwozesha binti kabla ya matokeo ya kidato cha nne kukiona cha moto
23 October 2023, 12:11 pm
Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wazazi kuwaozesha watoto wao baada tu ya kuhitimu masomo yao ya Sekondari bila kujari matokeo yatakuwa je, na wengine kuwapeleka mjini kufanya kazi za ndani jambo linalozorotesha ndoto za kielimu kwa mtoto wa kike.
Na: Elisha Magege.
Wazazi na walezi wilayani Sengerema wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kuozesha mabinti baada tu ya kuhitimu elimu ya sekondari na kuwakatishia ndoto zao za baadaye.
Akizungumza kwenye mahafali ya kidato cha nne shule ya sekondari Nyamazugo, mgeni rasmi ambaye ni diwani wa kata ya Tabaruka Mh. Sospeter Busumabhu amesema baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kukatisha ndoto za watoto wao kwa kuwaozesha na kuwafanyisha kazi za nyumbani.
Kwa upande wake Afsa Elimu kata ya Nyamazugo Bi. Jamila A. Magesa amesema pia kuna baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuwapeleka watoto wao kwa watu kufanya kazi za ndani na kwamba mzazi yeyote atakayebainika kufanya hivyo kabla ya matokeo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha mwenyekiti wa CCM kata ya Nyamazugo na mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho wamesema wamekuwa wakiwahimiza wazazi kupeleka watoto shule na wanaoshindwa kufanya hivyo huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Kata ya Nyamazugo ina jumla ya shule za sekondari 2 ambazo ni shule ya sekondari Kijuka na shule ya sekondari Nyamazugo ambapo kwa mwaka huu zimekuwa na wahitimu wa elimu ya sekondari 116 huku Kijuka ikiwa na wahitimu 42 na Nyamazugo 74.