Wananchi Buchosa walia na ubovu wa barabara
27 July 2023, 5:10 pm
Baadhi ya barabara kongwe nchini zimeonekana kutelekezwa na serikali ili hali zilitumika katika harakati za kudai uhuru wa taifa la Tanganyika zaidi ya miaka 60 iliyo pita.
Na: Katemi Lenatusi
Wananchi wa vijiji vya Busekeseke na Magulukenda katika kata ya Kalebezo halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza wanalazimika kuuza mazao ya nafaka na mazao ya mbao kwa bei ya hasara kwa zaidi ya miaka 17 kutokana na miundombinu mibovu ya rabaraba .
Wakizungumza na redio Sengerema kwa nyakati tofauti wananchi wa vijiji hivyo wamesema barabara hiyo inayotoka kijiji cha Kalebezo hadi Mkolani Geita ilikuwa kitovu cha usafirishaji lakini kwa sasa ni zaidi ya miaka 17 imepita barabara haijajengwa hivyo imepelekea shughuri za kiuchumi kukwama katika vijiji hivyo.
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Isaka Mashimba amekiri kuwepo kwa ubovu wa barabara hiyo na kwamba kwa bajeti ya mwaka 2023/2024 wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA wilayani Sengerema imetenga fedha shilingi milioni 200 ambazo zitajenga barabara yenye urefu wa kilometa 10 kutoka Magulukenda hadi kijiji cha Busekeseke.
Barabara ya Magulukenda hadi Busekeseke na Mkolani Geita licha ya kutokujengwa wala kufanyiwa ukarabati kwa miaka 17 lakini barabara hiyo itaendelea kukumbukwa kama miongoni mwa barabara zilizotumika kusaka uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.