Atuhumiwa kumbaka, kumpa ujauzito mwanae wa kambo
27 July 2023, 4:40 pm
Wimbi la watoto wa kike kubakwa katika Halmashauri ya Sengerema linazidi kushika kasi ambapo wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia wilayani hapo wamejitokeza na kulaani vitendo hivyo.
Na: Anna Elias
Mwanafunzi wa miaka 14 anayesoma darasa la saba katika shule ya msingi Nyampande anadaiwa kubakwa na kusababishiwa ujauzito na baba yake mlezi katika kijiji cha Nyampande wilaya Sengerema mkoani Mwanza.
Akieleza kwa uchungu mwanafunzi huyo amesema mama mzazi alisafiri na kumwacha na baba wa kambo ndipo alipotekeleza ukatili huo.
Redio Sengerema imemtafuta baba mzazi wa mtoto huyo ambapo amesema ametengana na mama mazazi wa mtoto huyo na kwamba badaye mama wa mtoto alimwomba mwanafunzi huyo aende kumsaidia kazi.
Aidha mama mzazi wa mwanafunzi huyo amekiri kubakwa kwa mtoto huyo huku akiiomba serikali kumchukulia hatua za kisheria mwanaume aliyehusika kufanya ukatili huo.
Kwa upande wao majirani wamelaani vikali kitendo cha mtoto huyo kubakwa na kusababishiwa ujauzito na kuiomba serikali kutoa adhabu kali kwa mhusika ili liwe fundisho kwa jamii.
Hata hivyo Redio Sengerema imemtafuta afisa mtendaji wa kijiji cha Nyampande Iddy Bundala ili kujua ofisi yake kama ina taarifa ya mwanafunzi kubakwa na kusema kuwa, amepata taarifa na tayari mtuhumiwa amefikishwa kituo cha polisi Sengerema.
Kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Nyampande Stephano Madoshi amekiri kupokea taarifa hiyo na kusema ni tukio la kwanza kutokea katika kijiji hicho huku akilaani kitendo hicho kwani mtoto huyo amekatishwa ndoto zake za kielimu.
Katibu wa SUMAUJATA Stela Mwakisalu amesema jamii inatakiwa kuwalinda watoto huku akiahidi kufuatilia tukio hilo ili mtoto huyo aweze kuendelea kupata haki za kielimu.