Akamatwa na jeshi la polisi kwa kumshushia kipigo mtoto mdogo
3 February 2023, 3:54 pm
Mama mlezi aliyemshambulia kwa kipigo kikali mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Msingi Bukala Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake kwa madai ya kukojoa kitandani hatimaye amekamatwa na jeshi la Polisi wilayani Sengerema.
Taarifa hiyo ya kukamatwa kwa mama huyo na jeshi la polisi imetolewa na afisa ustawi wa jamii katika kituo cha afya Sengerema Consolatha Magaka wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema kuwa tayari mama huyo amekamatwa na jeshi la polisi na kwamba mpaka sasa yupo mikononi mwa jeshi hilo kwa hatua zaidi za kisheria.
Baadhi ya wananchi wilayani humo wamepongeza hatua ya jeshi la polisi ya kumakamata mama huyo kwa kuwa litakuwa ni fundisho kwa akina mama wengine wenye tabia hiyo.
Viongozi wa dini wamewataka akina mama kuacha tabia ya kuwatesa watoto na badala yake wawalee katika maadili mema.
Naye afisa tathimini na ufuatiliaji kutoka taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Tuwajali inayojihusisha na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto Wilayani Sengerema John Kulindwa amepongeza jeshi la polisi na vyombo vya habari kwa kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili.
Ikumbukwe kuwa Januari 18 mwaka huu Radio Sengerema iliripoti habari ya Mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka saba anayesoma Darasa la kwanza katika shule ya Msingi Bukala Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ameshambuliwa kwa kipigo kikali na mama yake mlezi na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake kwa madai ya kukojoa kitandani.