Rais Samia afanya uteuzi wa wakuu wa mikoa,aikumbuka familia ya Nyerere.
15 May 2021, 2:36 pm
LEO Mei 15, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Makongoro Nyerere kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara akichukua nafasi ya Joseph Mkirikiti ambaye amehamishiwa mkoa wa Rukwa.
Makongoro ambaye ni mtoto Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi pia kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi mwaka 1995.
Makongoro anapata uteuzi huo ikiwa ni takribani miezi 10 baada ya kushindwa kwenye kura za maoni za CCM alipogombea ubunge wa Jimbo la Butiama pamoja na ndugu yake Madaraka Nyerere, ambapo Makongoro aliambulia kura 5 na Madaraka kura 2 kati ya 555 zilizopigwa, huku Jumanne Sagini akiibuka mshindi kwa kura 84 kati ya wagombea 59 waliojitokeza.
Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM na wadhifa mkubwa aliowahi kushika ni uenyekiti wa chama hicho katika Mkoa wa Mara 2007–2012, lakini pia Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, moja ya vikao muhimu ndani ya chama hicho.