DED Mwingine kupisha uchunguzi huko Buhigwe,Kigoma.
21 April 2021, 10:29 am
Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu amemsimamisha kazi mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Anosta Nyamoga kupisha uchunguzi.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Aprili 21, 2021 na kitengo cha mawasiliano serikalini imeeleza kuwa Ummy amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo kutoka kwa wananchi, viongozi na vyanzo vingine.
Waziri Ummy amemuagiza katibu mkuu wa Tamisemi, kupeleka timu ya uchunguzi mara moja na kumuelekeza mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuhakikisha timu hiyo inapata ushirikiano katika kipindi chote cha utendaji wao ili kumaliza kazi hiyo kwa wakati.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Buhigwe ndiyo anayotoka makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Philip Mpango, na jimbo hilo liko wazi mpaka sasa.
Jana Jumanne Aprili 20, 2021 Ummy alimsimamisha kazi mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Magesa Boniphace kupisha uchunguzi.
Taarifa ya Tamisemi ilieleza kuwa Boniphace alisimamishwa kazi baada ya Ummy kupokea malalamiko na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo kutoka kwa wananchi na viongozi mbalimbali akiwemo mbunge wa Sengerema (CCM), Hamisi Tabasamu.