Elimu bei elekezi ya vifurushi kizungumkuti.
2 April 2021, 11:53 am
Leo kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalumu imeanza kutumika Nchini ambapo wadau wameomba elimu izidi kutolewa juu ya kanuni hiyo mpya.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba aliahidi kuwa utekelezaji wa kanuni za kukabiliana na malalamiko juu ya huduma ya vifurushi zinazotolewa na kampuni mbalimbali za simu nchini utaanza Aprili 2, 2021.
Kanuni hizo ziliandaliwa kufuatia maoni 3,278 yaliyotolewa na wananchi kuhusu vifurushi hivyo ambapo baadhi ya mitandao ya simu jana iliwataarifu watumiaji wake juu ya hayo mabadiliko yanayoanza leo.
Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji TCRA, Dk Philip Filikunjombe alisema baadhi ya changamoto walizokuwa wakikutana nazo watumiaji wa huduma za simu ni pamoja na gharama za vifurushi kuwa juu na vifurushi vya data kubadilika mara kwa mara.
Hata hivyo baadhi ya watumiaji wa vifurushi wameiomba wizara ya mawasiliano na Tekinolojia ya habari pamoja TCRA kutoa elimu ya kutosha juu ya mabadiriko hayo kwani wengi walijua vifurushi vitashuka bei.