Orkonerei FM

Serikali yapunguza bei ya mbegu kwa 25%

23 February 2026, 1:57 pm

Na Dorcas charles

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Udhibiti wa Pembejeo, imetangaza punguzo la asilimia 25 ya gharama za mbegu ili kumpunguzia mzigo mkulima na kuongeza tija katika uzalishaji.

Picha ya afisa kilimo kata ya Terrat Simanjiro Bwana. Juma Mweka (picha na Isack Dickson)

Akizungumza katika mahojiano maalum, Afisa Kilimo wa Kata ya Terrat amewahimiza wakulima kufika katika ofisi yake kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni ili kusajiliwa na kupata namba ya ruzuku. Ili kunufaika na mpango huu, mkulima anapaswa kuwa na kitambulisho cha mpiga kura, kadi ya NIDA, au namba ya NIDA pekee, itakayomwezesha kununua mbegu ya aina yoyote kwa bei nafuu katika duka lolote nchini Tanzania.

Pamoja na unafuu huo wa bei, Afisa Kilimo huyo ametoa tahadhari kali kwa wakulima kuwa makini na ubora wa mbegu wanazonunua madukani. Amesisitiza kuwa ni lazima mkulima akague kifungashio ili kuhakikisha kina stika ya TOSCI (Mamlaka inayodhibiti ubora wa mbegu), tarehe ya kutengenezwa, na tarehe ya mwisho wa matumizi (expiry date). Aidha, amewashauri wakulima kuchunguza kama mbegu hizo zina usawa, hazijabunguliwa, wala kuchanganywa na uchafu wowote.