Orkonerei FM

Mzozo wa imani, mila Arusha, askofu Mwamba aanika chanzo

8 January 2026, 1:06 pm

Picha na Isack Dickson

Na Nyangusi Olesang’ida

Viongozi wa dini mkoani Arusha wameibua hofu juu ya mmomonyoko wa maadili na kupoteza sifa za kiroho kwa watumishi wa Mungu wanaojiingiza kwenye tamaduni za tohara za kienyeji ambazo zinakinzana na misingi ya kanisa.

Askofu Dr. Joel Mwamba, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Mitume mkoani humo, amebainisha kuwa mfumo wa sasa wa tohara za kimila unawaweka watumishi wengi njia panda, hali inayowafanya washindwe kurejea madhabahuni kutokana na vigezo vya kitamaduni vinavyowazuia kutekeleza majukumu yao ya kiroho baada ya kushiriki mila hizo.

Picha ya askofu Joel Mwamba

Askofu Mwamba ameyasema hayo mapema leo kwenye kipindi cha Amsha Amsha wakati akizungumza na Mwandishi wetu Nyangusi Olesang’ida na amesisitiza kuwa tatizo si tohara yenyewe bali ni mfumo unaotumika, huku akifichua kuwa tayari mazungumzo yameanza na uongozi wa kimila mkoani Arusha, chini ya kiongozi mkuu wa mila Tanzania.