Orkonerei FM
Orkonerei FM
4 September 2025, 6:57 am

Na Mwandishi Wetu
Simanjiro, Manyara – Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Ndg. Gracian Makota, ameshiriki kikao cha utafiti wa magonjwa yanayoambukizwa kwa mfumo wa hewa kilichofanyika katika Kata ya Mirerani, wilayani Simanjiro, kikilenga kuelimisha jamii kuhusu namna magonjwa hayo yanavyoenea na athari zake.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali na binafsi, ambapo mada kuu ilihusu usalama wa afya kwa jamii inayoishi na kufanya kazi katika mazingira hatarishi, hususan wachimbaji wa madini ya Tanzanite.
Akiwasilisha hoja yake, Dkt. Alexander William, mtafiti kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Matibabu cha Kikristo Kilimanjaro (KCMC) na daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Kibong’oto, alisema watu walio hatarini zaidi kuugua kifua kikuu (TB) na silicosis ni wale wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji madini kutokana na kuvuta vumbi linalotokana na ulipuaji wa baruti migodini.
Dkt. William alishauri wachimbaji kuchukua tahadhari madhubuti za kiafya ikiwemo matumizi ya maji kwenye shughuli za uchimbaji ili kupunguza wingi wa vumbi. Pia, alisisitiza kuwa ni muhimu kuendelea na tafiti zaidi zitakazosaidia kudhibiti na hatimaye kutokomeza magonjwa haya miongoni mwa wachimbaji nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Makota aliwataka wadau wote kuunga mkono jitihada za wataalamu wa afya na serikali katika kulinda ustawi wa jamii, hasa katika maeneo yenye shughuli kubwa za madini.