Orkonerei FM

Madereva 800 wapatiwa mafunzo maalum msimu wa utalii Arusha

30 May 2025, 2:56 pm

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP William Mkonda akizungumza mbele ya Madereva mkoani Arusha. (Picha na Nyangusi Ole Sang’ida)

Jeshi la Polisi limeendesha mafunzo kwa madereva 800 wa magari ya utalii Arusha, kuelekea msimu wa utalii ili kuhakikisha sheria za barabarani zinafuatwa na usalama wa watalii unaimarishwa.

Na Nyangusi Ole Sang’ida

Zaidi ya madereva 800 wa magari ya utalii mkoani Arusha wamepatiwa mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, ikiwa ni maandalizi ya msimu wa utalii (high season) unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akifungua mafunzo hayo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) William Mkonda, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha madereva sheria, kanuni na matumizi sahihi ya barabara ili kuhakikisha usalama wa watalii unaimarishwa, na hivyo kuitangaza vyema Tanzania kama taifa salama.

Sauti ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) William Mkonda

Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Watalii nchini (TTGA), Bw. Lembrisi Moses, amesema kuwa madereva hao wamejengewa uwezo mkubwa kupitia mafunzo hayo, huku akieleza kuwa wamekumbushwa umuhimu wa kuzingatia alama za barabarani na mwendo sahihi.

Sauti ya Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Watalii nchini (TTGA), Bw. Lembrisi Moses

Naye mmoja wa madereva walioshiriki mafunzo hayo, Bw. Usia Israel, amesema kupitia elimu hiyo wamejifunza kuhusu udereva wa kujihami ambao utasaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo zinaweza kuepukika.

Sauti ya Usia Israel mmoja wa madereva waliopata mafunzo

Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa Jeshi la Polisi katika kuwajengea uwezo madereva wa makundi mbalimbali ili kuhakikisha usalama unatawala kwenye sekta ya utalii nchini.