Sukuro wapanda juu ya mti kupata mawasiliano
12 October 2024, 10:56 am
Je, umewahi kufikiria maisha ambayo kila unapohitaji kuwasiliana na familia yako ni lazima upande juu ya mti ili upate mtandao?
Na Isack Dickson
Katika kijiji cha Sukuro kilichopo kata ya Komolo, wilaya ya Simanjiro, mawasiliano ya simu si jambo rahisi. Kila siku, wananchi wa kijiji hiki wanapambana na changamoto ya mtandao hafifu wa simu, hali inayowalazimu kupanda juu ya miti ili kupiga simu au kutuma ujumbe. Katika sehemu nyingine, huduma za kutuma na kupokea pesa, ambazo zinahitaji mtandao, zimegeuka kuwa safari hatari, kwani wakala wa huduma hiyo hulazimika kupanda juu ya mti ili kuhudumia wateja wake.
Kwa wakazi wa Sukuro, mawasiliano yamekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo na usalama. Wakazi, wanaelezea jinsi wanavyolazimika kutumia mbinu za kizamani na zenye hatari ili kufanikisha mawasiliano yao na ndugu zao walioko mbali.
Katika mazungumzo chini ya mti ambao ni sehemu pekee inayopatikana mtandao, wakazi wa kijiji hiki wameelezea hali yao kwa uchungu, wakionyesha matumaini ya kuwa siku moja, suluhisho la kudumu litapatikana. Mtendaji wa kijiji ameeleza hatua ambazo serikali ya kijiji imejaribu kuchukua ili kutafuta msaada wa kiteknolojia na kufanikisha upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika kwa wananchi.