Uzinduzi soko la kijiji cha Engonongoi wilaya ya Simanjiro
20 February 2024, 3:28 pm
Wakaazi wa kijiji cha Engonongoi iliyopo kata ya Terrat wilaya ya Simanjiro wameungana na wananchi wenzao na wafanyabiashara kutoka vijiji vya wilaya ya Simanjiro na wilaya za jirani katika ufunguzi wa soko katika kijiji cha Engonongoi.
Na Baraka David Ole Maika.
Tukio hilo la kihistoria katika kijiji cha Engonongoi lilifanyika jana Jumatatu Februari 19, 2024 katika kitongoji Loordekes katika kijiji cha Engonongoi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama, serikali, makanisa na viongozi wa mila kutoka ndani na nje ya kata ya Terrat.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa soko hilo litakalokuwa likifanyika kila siku za Jumatatu, mwenyekiti wa kijiji cha Engonongoi Bw. Nemamiyai Shinini amesema kuwa kuanzishwa kwa soko hilo itawezesha wananchi kupata huduma kwa karibu kwani wamekuwa wakienda umbali mrefu kwa ajili ya minada.
Naye mwenyekiti wa CCM kata ya Terrat ndugu Soipei Koromo amewasihi viongozi wa kijiji cha Engonongoi kuwapa kipaumbele akinamama kwa kuwapatia maeneo ya kufanyia biashara katika soko hilo.
Aidha mgeni rasmi katika ufunguzi wa soko hilo diwani wa kata ya Terrat mh Jackson Materi amesema kuwa soko hilo ni fursa kwa wakazi wa kijiji cha Engonongoi na vijiji vya jirani.
Soko hilo la kijiji cha Engonongoi linatazamiwa kuwaunganisha wafanyabiashara na wananchi kutoka kata za Terrat, Oljoro namba 5, Emboreet za wilaya ya Simanjiro pamoja na kata ya Lemooti, Lokisale na Moita za wilaya ya Monduli.