Micheweni FM

RC kaskazini Pemba awataka vijana kutumia fursa  mitandao ya kijamii

11 November 2026, 2:53 pm

Picha ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abdallah Rashid Ali na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Pemba, Said Mussa Rashid wakiwa katika ya pamoja Picha na Essau Kalukubila.

mradi wa kuwajengea uwezo vijana katika matumizi sahihi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, unaotekelezwa na Jumuiya ya Vijana Pemba

Na Essau Kalukubila.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya, amewataka vijana kuitumia vyema mitandao ya kijamii kwa kutafuta fursa mbalimbali za maendeleo na kujiongezea kipato, badala ya kuitumia vibaya kwa kuvunja sheria za nchi.

Ameyasema hayo wakati akifungua rasmi mradi wa kuwajengea uwezo vijana katika matumizi sahihi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, unaotekelezwa na Jumuiya ya Vijana Pemba, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Vijana Weni, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema maendeleo ya teknolojia yamefungua milango mingi ya kiuchumi kwa vijana, hivyo ni wajibu wao kutumia mitandao ya kijamii kwa ubunifu, biashara na kutafuta maarifa yatakayowawezesha kujitegemea.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya

Sambamba na hayo, Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abdallah Rashid Ali, amesema mafunzo hayo yanapaswa kuwa chachu kwa vijana kutumia mitandao ya kijamii kama nyenzo ya kuwaunganisha na fursa mbalimbali za ajira, biashara na maendeleo zinazopatikana ndani na nje ya Pemba.

Ameeleza kuwa matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kusaidia kupunguza changamoto za ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abdallah Rashid Ali

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Pemba, Said Mussa Rashid, amesema mradi huo umeanzishwa baada ya utafiti kubaini kuwa vijana wengi wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii bila kuwa na malengo mahsusi yanayoweza kuwaletea manufaa.

Naye Salum Mwinyi Juma, aliyemwakilisha Mratibu wa Vijana Pemba, amesema ipo fursa kubwa ya vijana kujifunza, kufanya biashara na kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii ikiwa watatumia majukwaa hayo kwa njia sahihi.

Sauti ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Pemba, Said Mussa Rashid na Salum Mwinyi Juma, aliyemwakilisha Mratibu wa Vijana Pemba

Mradi huo unatarajiwa kuwajengea vijana uwezo wa kutumia teknolojia ya mawasiliano kwa tija na kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali za kijamii na kiuchumi zinazopatikana kupitia mitandao ya kijamii.