Micheweni FM
Micheweni FM
13 October 2026, 6:42 pm

mafunzo hayo yamejikita zaidi kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, lengo ni kuwapa ujuzi wa kitaalamu utakaowasaidia kuboresha ufugaji na kuongeza uzalishaji wa maziwa
Na Essau Kalukubila.
Katika kuendeleza elimu na ujuzi kwa wafugaji, Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar imetoa mafunzo kwa wafugaji yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu bora za ufugaji ili kuongeza uzalishaji na kufanya shughuli hiyo kuwa na tija kiuchumi.
Afisa kutoka Idara ya Maendeleo ya Mifugo, Kitengo cha Elimu kwa Wafugaji, Zehra Karim Zam, amesema mafunzo hayo yamejikita zaidi kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, lengo ni kuwapa ujuzi wa kitaalamu utakaowasaidia kuboresha ufugaji na kuongeza uzalishaji wa maziwa.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo wamewataka wafugaji kuzingatia utaratibu wa kuhifadhi majani na malisho ya mifugo ili yatumiwe wakati wa kiangazi, hatua itakayosaidia kukabiliana na upungufu wa malisho na kudumisha uzalishaji wa maziwa kwa kipindi chote cha mwaka.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo waliyoyapata, wakieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia kuboresha mbinu zao za ufugaji, kuhifadhi malisho kwa wakati na kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa.
Mafunzo hayo ni sehemu ya maonesho ya Siku ya Chakula yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe, yakilenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya uzalishaji wa chakula na kuhamasisha matumizi ya mbinu bora za ufugaji.

Afisa kutoka Idara ya Maendeleo ya Mifugo, Kitengo cha Elimu kwa Wafugaji, Zehra Karim Zam akizungumza katika mafunzo ya kuwapa elimu wafugaji katika maonyesho ya chakula Duniani yanayofanyika Chamanangwe Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba Picha na Essau Kalukubila.