Micheweni FM

Mpambani Kojani wawapa tano polisi jamii

2 October 2023, 1:08 pm

Mwonekano wa kisiwa cha Kojani wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba. Picha na Mwiaba Kombo

Kojani ni miongoni mwa kisiwa ambacho kinapatikana upande wa Mashariki mwa kisiwa cha Pemba mkoa wa Kaskazini Pemba wilaya ya Wete.

Na Mwiaba Kombo

Wananchi  wa wilaya ndogo Kojani shehia ya Mpambani wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba, wameishukuru polisi jamii yao, kwa kudhibiti na kukabiliana na vitendo vya kihalifu kijijini hapo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, wananchi hao wamesema, tokea kuanzishwa kwa ulinzi shirikishi shehiani hapo, vitendo vya kihalifu vimepungua.

Wamesema kuwa, ulinzi shirikishi umekuwa mwarobaini tosha katika kijiji chao, kwani umeupunguza matendo maovu, jambo ambalo kabla ya hapo halikuwepo.

Wananchi hao wameeleza kuwa, umoja na mshikamano uliopo, umesaidia kudhibiti vitendo viovu, kama vile wizi wa mazao na mifugo, na kupelekea kuishi kwa amani na utulivu.

Mmoja kati ya wananchi hao Said Haji Said amesema, kwa sasa mifugo na vipando vyao vinanawiri, kutokana na kuimarika kwa ulinzi shirikishi, kijijini kwao.

Amesema kwa sasa wafugaji, na wakulima wanavuna wanachokipanda kwa wakati, kutokana na kuimarika kwa ulinzi shirikishi, jambo ambalo halikuwepo kwa muda mrefu kijijini kwao.

Nae Fatma Nassor Ali ameeleza kuwa, kuimarika kwa ulinzi shirikishi kijijini kwao, imetoa fursa kwa wanawake na watoto, kutembea bila ya wasiwasi hasa nyakati za usiku wamapema wanapokuwa na shughuli zao.

Aidha Mwanakame Kombo Hassan, amesema kilichobakia kwao, ni kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu na kikundi cha ulinzi shirikishi, katika kuiweka shehia yao salama.

Mapema Mjumbe wa polisi jamii shehiani hapo, Othman Mwinyi Shezume alisema,  polisi jamii imekuwa ikifanya kazi zake ipasavyo, ili kudhibiti vitendo vyote vya kihalifu, kijijini hapo, kama vile wizi, ubakaji uporaji na utoro wa watoto masomoni.

Alieleza kuwa, wamefanikisha majukumu yao hayo, na yameleta mafanikio makubwa, kutokana na kuwepo kwa ushirikiano mzuri, baina yao na wanakijiji wa shehia hiyo.

Kwa upande wake Naibu Sheha wa shehia hiyo Hassan Iddi Othman, amewaomba wanakijiji wa shehia ya Mpambani, kuzidi kuleta ushirikiano na polisi jamii, ili kuunga mkono juhudu zao kwa lengo la kufanikisha azma yao.

Hata hivyo ameiomba, serikali kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu na polisi jamii hiyo, juu ya changamoto ambazo wanapitia wakati wa utendaji wa kazi zao, kwa kuwapa mafunzo maalum.