Micheweni FM

IGP Ussi awataka Wete kutochimba vyoo, karo kwenye vyanzo vya maji

24 November 2023, 9:46 am

Insepekta Khalfan akizungumza na maimamu na walimu wa madrasa katika shehia ya mjananza wilaya ya wete mkoa wa kaskazini Pemba

Choo ni moja kati ya jambo muhimu katika nyumba hivo ni muhimu kuhakiksha kila mwanajamii amechimba choo katika nyumba yake lakini licha ya umuhimu wake ni lazima kuhakiksha huchimbi choo hicho karibu na vianzio vya maji kwani vinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi.

Na Zuhura Juma

Wananchi kisiwani Pemba wametakiwa kuacha tabia ya kuchimba mashimo ya vyoo na makaro karibu na vyanzo vya maji, ili kuepusha uchafuzi wa maji ambayo yanaweza kusababisha maradhi ya kuharisha.

Akizungumza na masheikh, maimamu na walimu wa madrasa katika shehia ya Mjananza wilaya ya Wete Pemba, Inspekta wa Jeshi la Polisi Khalfan Ali Ussi amesema kuwa, kipindi hiki ni cha mvua  wananchi wachukue tahadhari kujiepusha na madhara mbalimbali ikiwemo maradhi ya mlipuko na maafa.

Amesema kuwa, ni vyema viongozi wa dini wakachukua juhudi ya kuwaelimisha wananchi waache kuchimba mashimo ya vyoo na makaro kwenye vianzio vya maji, kwani ndiyo wanayotumia kwa kunywa na kupikia, hivyo yanaweza kuchafuka na kuwasababishia maradhi.

Ameeleza kuwa, pia wanatakiwa kufunika makaro yao ili yasiweze kusababisha madhara ikiwemo vifo, kwani wakati wa mvua watoto wanacheza sehemu wasizozijua na hatimae wanaweza kutumbukia.

Amewataka viongozi hao wa dini, kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe ujumbe huo unawafikia wananchi kabla ya kutokea madhara, kwani wao wanakaa na watu wengi kwa wakati mmoja na wanaaminiwa sana na jamii

Sambamba na hayo ameitaka jamii kushirikiana pamoja na  kuimarisha ulinzi maneno yote sambamba na kuendelea kumtumia vikundi vya ulinzi shirikishi kuimarisha doria hasa nyakati za usiku.

Vile vile amewaasa wananchi kusikiliza, kufuatilia na kutekeleza taarifa na maelekezo ya wataalamu wa hali ya hewa ili kuepuka maafa masiyo ya lazima.

Kwa upande wao viongozi wa dini wamesema kuwa, elimu waliyopewa wataifanyia kazi kwa maslahi ya jamii na taifa, huku wakiahidi kuwafikishia wananchi ili waweze kujikinga na madhara mbali mbali yanayoweza kujitokeza wakati mvua zikiandelea.