Micheweni FM

ZATU yaiomba serikali kuwepo tume ya utumishi ya walimu Zanzibar

5 October 2023, 3:43 pm

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdalla Said akifungua kongamano la siku ya walimu duniani katika ukumbi wa chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA) Wete Pemba picha na Mwiaba Kombo

Elimu ni haki ya kila mtu hivyo kila mmoja kwa mujibu wa nafasi yake hana budi kuhakikisha anashirikiana kwa pamoja na wenzake ili watoto waweze kupata haki yao ya msingi ya elimu.

Na Mwiaba Kombo.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imekihakishia Chama Cha cha Walimu Zanzibar (ZATU) kushirikiana kwa pamoja katika kutatua changamoto  mbalimbali zinazowakabili katika sekta ya hiyo.

Akifungua kongamano la siku ya walimu duniani katibu mkuu  wa wizara hiyo Zanzibar Khamis Abdalla Said kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanziba  Lela Mohammed Mussa amesema ni  haki ya kila mwalimu kuhakikisha anapata stahiki zake zote ambazo anastahiki .

Amesema wapo baadhi ya walimu wakuu wameshindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo ,hivyo ni vyema kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika majukumu yake .

Aidha amewaomba walimu ambao bado hawajajiunga na ZATU kuhakikisha wanajiunga na chama hicho ili waweze kutatuliwa kero zao kwa haraka .

Akitoa salamu za Wizara ya Elimu Pemba afisa mdhamini wa wizara ya elimu Pemba Mohd Nassor Salim amesema zaidi ya walimu 1446 wameajiriwa katika kisiwa cha Pemba kuanzia mwezi Januari mpaka sasa hivyo ni jukumu la walimu kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi zaidi.

Amesema bado matokeo ya kidato cha nne hayaridhishi kwa mikoa yote miwili Kaskazini na Kusini Pemba hivyo ni jukumu la kila mmoja kwa nafasi yake kusimamia ili wanafuzi waweze kufanya vizuri.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Zanzibar  wa Chama Cha Mapinduzi Mohd Said Dimwa ameitaka serikali kuhakikisha inafanya mchakato haraka wa kupatikana tume ya utumishi ya walimu Zanzibar kabla ya mwaka huu kumalizika.

Ameeleza kuwa lengo la Rais wa Zanzibar ni kuona Pemba inafunguka kama sehemu zingine kutokana na neema ambayo inapatikana kisiwani hapa.

Akisoma risala ya walimu kwa mgeni rasmi Katibu Mkuu wa ZATU Haji Juma Omar ameiomba serikali kurejesha nauli za walimu ambao wanaishi mbali na maeneo ya kazi ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi .

Chama cha walimu Zanzibar kimeadhimisha siku ya walimu duniani katika ukumbi wa chuo kikuu Zanzibar SUZA Wete kwa kauli mbiu isemayo ,kuwepo kwa tume ya utumishi ya walimu Zanzibar, kutatatua changamoto zinazowakabili walimu wa Zanzibar.