Micheweni FM

Maafisa kilimo Zanzibar wapewa rai

24 August 2023, 7:29 am

Mkuu wa Tathmini na Ufatiliaji kutoka mradi wa viungo Ali Abdalla Mbarouk akiwasilisha mada ya matumizi bora ya kilimo kwa washiriki wa mradi wa viungo ambao hawapo pichani(picha Nafda Hinid)

Mradi wa viungo ni mradi ambao umekuja kwa lengo la kumkomboa mwananchi kiuchumi kuondokana na hali ngumu ya maisha.

Na Mwiaba Kombo

Maafisa kilimo wameshauriwa kutoa taarifa kamili kuhusu udongo bora wenye kukidhi viwango kwa lengo la kuzalisha mazao bora kwa wakulima.

Hayo yameelezwa  na mkuu wa tathmini na ufatiliaji kutoka mradi wa viungo Ali Abdalla Mbarouk katika  kikao cha pamoja  kilichowashirikisha wadau wa mradi huo chenye lengo la kujadili mbinu bora na mikakati imara ya kuendeleza kilimo chenye tija kwa wakulima kilichofanyika jengo la benki ya watu wa Zanzibar katika ofisi za mfuko wa bima .

Amesema ipo haja kwa Wizara ya Kilimo kufanya tathmini kwa wakulima kwa kila wilaya kugundua changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka ikiwemo kutokufahamu udongo sahihi kwa matumizi bora ya kilimo.

Naye mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya mradi wa viungo (ZMAG) ambaye pia ni mkurugenzi Sera, Mipango na Kilimo Makame A. Makame amesema kwa sasa ipo haja kwa Zanzibar kuuza bidhaa zilizochakatwa nje ya nchi  badala ya mali ghafi kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao yanayotoka nchini

Mkuu wa mawasiliano  kutoka mradi wa viungo Sophia Ngalapi amesema mradi wa viungo umekuja kuwakomboa wakulima hivyo zinahitajika mbinu mbadala zitakazowasaidia wakulima kusonga mbele katika kulima kilimo chenye tija na kubadili maisha yao,

Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho wamesema pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kujenga masoko mbalimbali katika visiwa hivyo kwa sasa wanahitaji soko la bidhaa za kilimo hai kujitegemea badala ya kuchanganywa na masoko mengine.

Mkutano huo wa nane wa kujadili masuala mbalimbali ya utekelezaji wa mradi na kushauri njia mbadala ili kufikia malengo ya mradi wa viungo Zanzibar unaotekelezwa na TAMWA ZNZ, Community Pemba Forest (SPF) na People Development Forum (PDF) ni mradi wa miaka minne ambao uko chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Umwagiliaji Zanzibar unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.