Micheweni FM

Wakulima, wafugaji Kojani wanyoosheana vidole

13 August 2023, 2:13 pm

Mkulima wa Kojani akikata mbegu za mhogo baada ya shamba lake kuharibiwa na wanyama(picha na Mwiaba Kombo)

Baada ya migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji katika shehia ya Kojani bado suala hili limekuwa kizungumkuti kutokana na kukosekana kwa ufumbuzi wa tatizo hilo.

Na Mwiaba Kombo

Wakulima shehia ya Kojani Wilaya ndogo ya Kojani mkoa wa Kaskazini Pemba, wamewalalamikia wafugaji kutodhibiti mifugo yao, jambo ambalo hupelekea uharibifu wa mazao yao.

Akizungumza na Micheweni Fm, mkulima wa Viazi vitamu Saada Ali Faki kijijini hapo, amesema wamekua wakijishughulisha na kilimo ili kujikwamua kiuchumi, ingawa wafugaji hurejesha nyuma jitihada zao.

Amesema wamekuwa wakitumia nguvu na gharama kubwa, kupanda mazao ili yawasaidie kiuchumi, ingawa malengo yao hayafikiwi kwani wafugaji hushindwa kudhibiti mifugo yao na kufanya uharibifu mkubwa.

Nae mkulima wa zao la Mtama Bikombo Said Hamad amesema, wamekua wakichukua hatua kadhaa, ili kudhibiti suala hilo ikiwemo kuripoti matukio hayo kwa uongozi wa shehia na hatua stahiki kuchukuliwa, ingawa bado suala hilo linaendelea kijijini kwao.

Akizungumzia kadhia hiyo, mfugaji wa Ng’ombe na Mbuzi, Hassan Hussein Makame amesema, kuna haja kubwa kwao kudhibiti mifugo yao ili kuzuia uharibifu unaotokezea.

Katika hatua nyingine amewaaasa wakulima, kutolinyamazia suala hilo, na ni muhimu kuliripoti katika vyombo vya sheria, ili wafugaji wasiodhiti mifugo yao kuchukuliwa hatua.

Nae mfugaji wa Mbuzi Issa Mohamed Yakoub, alisema wamekuwa wakiidhibiti, ingawa uharibifu mwengine unatokea, pale wanapokata kamba.

Kwa upande wake naibu sheha wa shehia hiyo Ali Hamad Ali, ameeleza kuwa  amekua akipokea malalamiko mara kwa mara kutoka kwa wakulima, juu ya wafugaji kutodhibiti mifugo yao, na tayari wameshachukua hatua kadhaa, kama kuzungumza na wafugaji.

Hata hivyo amewataka wakulima kufanya mazungumzo ya utatuzi wa migogoro baina yao na wafugaji na wajiepushe na kujichukulia sheria mikononi.

Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakari, amesema  kuwa wilaya itaendelea kuwatuma wataalamu na kutoa elimu ya kukinga na migogoro inayoepukia.